Njia 5 za Kushinda Kuahirisha

Soma posti hii kwa dakika 3 (makadirio)

Baada ya kuangalia sehemu ya kwanza na ya pili ya mfululizo huu, leo tumalizie kwa kuangalia sehemu ya tatu na ya mwisho.

Katika posti mbili zilizopita tuliangalia tatizo la kuahirisha kwa ujumla na vyanzo vyake.

Leo tuangalie njia za kushinda kuahirisha, njia ambazo zinatokana na kile tunachokijua juu ya saikolojia ya tatizo hili.

1. Kupanga Kujizawadia Pale Usipoahirisha (Self-Reinforcement)

Wakati unapanga mpango fulani pia panga zawadi utakayojipatia pale utakapofanikiwa kuutekeleza.

Mfano mpango wako ni kufanya mazoezi kwa nusu saa kila siku. Pia ni mtu unayependa sana kuingia Instagram.

Unapotumia njia hii utaweza kuingia Instagram pale tu utakapomaliza kufanya mazoezi kwa siku husika – ukishindwa kufanya mazoezi, hakuna Instagram!

Kwa kutumia njia hii unaulazimisha ubongo kukithamini kitendo cha kufanya mazoezi SASA (japo faida ya kitendo hiki iko miaka mingi ijayo – na siyo sasa) kwa kuwa kinahusiana na faida ya SASA ya kuingia Instagram – na hivyo kushinda kuahirisha.

2. Kutengeneza Mazingira ya Kutoahirisha (Commitment Devices)

Njia hii inaondoa mazingira yote yanayochochea kuahirisha. Kwa maneno mengine inaongeza ugumu wa kuahirisha.

Mfano mpango wako ni kumaliza kusoma kitabu cha Prayer Driven Life mwezi huu. Kitabu hiki kiko katika softcopy.

Kila mara unapoanza kukisoma umekuwa ukijikuta unaishia kuahirisha na badala yake kuangalia movies zilizoko kwenye laptop unayoitumia.

Unapotumia njia hii ni ama utafuta movies zote kwenye hiyo laptop unayoitumia ama utahamisha kitabu hiki na kukiweka kwenye laptop isiyo na movies.

Mazingira yanayotengenezwa kwa lengo hili wanasaikolojia wanayaita ‘Commitment Device‘.

Na njia hii tunaitumia mara nyingi katika maisha yetu ya kila siku, mfano: kwenye mifuko ya jamii (mfanyakazi anaondolewa uwezo wa kuamua kutoweka akiba kwa ajili ya maisha ya baadae); kuzuia upatikanaji wa tovuti za mitandao ya kijamii katika sehemu za kazi (kuondoa mazingira yanayochochea kuahirisha kufanya kazi); n.k.

3. Kufanya Iwe Rahisi Kuanza Jambo

Pamoja na ‘time inconsistency’ sababu nyingine kubwa ya kuahirisha huwa ni ugumu ulioko katika kuanza kufanya jambo.

Mara nyingi ni vigumu zaidi kuanza kufanya jambo kuliko ilivyo katika kuendelea nalo.

Kufanya kitendo cha kuanza kufanya jambo kiwe rahisi na kifupi kadri inavyowezekana kutaleta urahisi katika kuanza kufanya jambo na hivyo kutoliahirisha.

Njia mojawapo ya kushinda kuahirisha ni kuligawa jambo hilo katika sehemu ndogo ndogo zinazoweza kutekelezeka ndani ya muda mfupi.

Mfano, inaweza kuwa unachotaka kufanya ni kuandika kitabu; kazi hii unaweza kuivunja katika sehemu ndogo ndogo kama kuandika maneno 200 kwa siku.

Utaona ni rahisi sana kuahirisha unapofikiria kazi husika kuwa ni kuandika kitabu, kuliko ilivyo pale unapofikiria kazi ni kuandika maneno 200 kwa siku.

4. Kuleta Athari ya Kuahirisha (iliyokuwa ipatikane siku za mbeleni) SASA

Kwa kuwa ubongo unapofanya maamuzi unajali zaidi faida/hasara ya sasa kuliko ilivyo kwa ya baadae, basi ukiweza kuhusianisha hasara ya SASA na kitendo cha kuahirisha utausaidia ubongo wako kufanya maamuzi yatakayojaribu kushinda kuahirisha.

Mfano kila wakati umekuwa ukiahirisha kuweka akiba – ambayo unajua itakufaa wakati wa uzeeni – na badala yake umekuwa ukiitumia pesa hiyo kununua mavazi na kufanyia starehe (vitu ambavyo vinaleta raha/faida SASA lakini vinavuruga na kuondoa uwezekano wa kupata faida uzeeni ambayo ingetokana na kuweka akiba).

Ukiwaambia rafiki zako kadhaa juu ya mpango wako wa kuweka akiba kila mwisho wa mwezi na kuripoti kwao, inapofika mwisho wa mwezi itakuwa ngumu kuahirisha kwa kuwa ubongo utakuwa unaogopa aibu ya kuonekana muongo, mbabaishaji na mtu asiyesimamia maneno yake (hasara ya SASA) pale utakapoahirisha.

Njia nyingine ni ya kutumia app inayoitwa stickK ambapo baada ya kujisajili unaweka kiwango cha pesa ambacho utakatwa pale utakapoahirisha – kiwango hicho kitaenda katika taasisi za kusaidia wasiojiweza.

5. Kuongeza Madhara Yatakayopatikana kwa Kuahirisha

Wakati mwingine ni rahisi kwa ubongo kuahirisha kwa kuwa ukiangalia madhara unaona ni madogo, yanakuja taratibu na tena ndani ya muda mrefu.

Kwa hiyo ukiweza kuufanya ubongo uone madhara makubwa ya kuahirisha, tena ndani ya muda maalumu unaoeleweka waziwazi basi itakuwa vigumu kuahirisha.

Mfano wewe ni mwanamuziki, na umepanga hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu uwe umetoa albamu mpya.

Pale utakapotangaza kwa mashabiki wako tarehe rasmi ya uzinduzi wa albamu hiyo, na tena ukalipia kabisa ukumbi utakaotumika kwa uzinduzi huo, itakuwa vigumu sana kwako kuahirisha mpango wako wa kutoa albamu mpya ndani ya mwaka huu.

Hii ni kwa sababu kila utakapokuwa ukifikiria kuahirisha kufanya mazoezi ya kutengeneza nyimbo picha ya hasara kubwa utakayoipata kwenye ukumbi na tena aibu kwa mashabiki wako itakuwa halisi kiasi cha kuufanya ubongo uione kuwa ni ya SASA na hivyo uweze kushinda kuahirisha.


Je, kuna njia yoyote ambayo huwa unaitumia ili kushinda kuahirisha? KARIBU utushirikishe kwenye comments ili tujifunze zaidi…

0 comments