Nimechoka Kuahirisha

Soma posti hii kwa dakika 3 (makadirio)

Email inaingia kwenye inbox yangu, kichwa chake kinasema, ‘Your domain nilichojifunza.com expires in 29 days’, ikimaanisha anwani ya mtandao ya tovuti yangu ya nilichojifunza.com inafikia muda wa mwisho wa matumizi baada ya siku 29. Kwa maneno mengine napaswa kulipia anwani hiyo ndani ya siku 29 ili tovuti hii iendelee kupatikana mtandaoni.

Anwani hii hulipiwa kila baada ya miezi 12, kwa hiyo mara ya mwisho kuilipia ilikuwa mwaka mmoja uliopita lengo likiwa ni kuwa na tovuti ambayo ningeitumia kushirikisha yale ninayojifunza kila siku.

Lengo la pili lilikuwa ni kupata sehemu nitakayoitumia kama uwanja wa mazoezi ya uandishi; ikiwa ni sehemu ya mipango niliyoipanga ya kufikia lengo la kuandika vitabu siku moja.

Kwa mwaka huu wote unaoisha kila siku nimekuwa nikiishia kuahirisha na kujiambia nitaanza kuandika hivi karibuni ‘nitakapopata nafasi’, pale ubize utakapopungua.

Nilijiambia hivyo siku nilipoiweka nilichojifunza.com hewani, nikajiambia tena siku iliyofuata, na tena siku iliyofuata, hatimaye ikawa wiki!

Nikajiambia tena wiki iliyofuata, na tena iliyofuata, hatimaye ikawa mwezi! Zoezi likajirudia kwa mwezi wa kwanza, kisha wa pili, wa tatu, hatimaye leo wa 12; na bado hiyo ‘nafasi’ haijapatikana, na huo ubize haujapungua – tena umeongezeka!

Unaweza kudhani labda ni kwa sababu uandishi si kitu rahisi, lakini stori ni hiyo hiyo hata katika maeneo mengine: Moja ya malengo yangu ya kikazi ilikuwa ni kunoa ujuzi wangu wa graphics design na mpango ukawa ni kila siku ku-design kazi moja na ku-share mtandaoni, na unajua kilichotokea? Yap, ni hicho hicho unachofikiria – hadi leo bado nasubiri ‘kupata nafasi’!

Pia mwanzoni mwa mwaka huu nilijisajili uanachama wa maktaba na nikapanga ratiba ya kuhudhuria mara mbili kila wiki; Mwezi ujao wa Januari naenda kupyaisha uanachama wangu tena, na hiyo itakuwa ni mara ya pili kuingia katika maktaba hiyo, mara ya kwanza ikiwa ni pale nilipoenda kujiunga mwanzoni mwa mwaka huu!

Orodha inaweza kuendelea na kuendelea, lakini kwa leo haya maeneo matatu yanatosha kuelezea tatizo nililonalo la kuahirisha – na ukubwa wake.

Na hata hii posti unaweza kudhani nimeiandika kwa dakika ama saa chache tu, lakini ukweli ni kwamba imenichukua siku 38 kuikamilisha; si kwa sababu ilihitaji uchunguzi na uchambuzi wa kina kiasi hicho, la – kama unavyoona imejaa stori tu – bali kwa kuwa muda niliopanga kuutumia kuiandika niliona ‘sina nafasi’ kwa hiyo nikaazimia kuiandika ‘nitakapopata nafasi’; ama katika huo muda ‘niliopata nafasi’ baada ya kuiandika kwa dakika mbili nikaona acha ni-google tafsiri ya neno ‘graphic’ kwa Kiswahili, halafu baada ya kuikosa (hivi unajua eti haipo!?) nikaamua kutafuta historia ya Elon Musk, nikaipata kwenye Wikipedia, nilipoisoma hadi nusu nikataka kujua na ya makampuni yake Tesla na SpaceX – kwa hiyo nikafungua Wikipedia zao, baada ya kumaliza kusoma hizo historia zote nikahisi nimechoka kwa hiyo nikaamua kujilaza nipumzike, basi kwa muda huo ndo ikawa imeishia hapo tena…nikawa nimeamua kuahirisha!

Unaweza kusema sipendi kutimiza kile nilichopanga, na tena siko siriasi, lakini ukweli ni kwamba napenda na natamani sana kutimiza kile nilichopanga, tena niko siriasi na ndio maana nikalipia website kuwa hewani na nikaitengeneza, nikajisajili uanachama wa maktaba, n.k.

Kwa hiyo ukisema siko siriasi utakuwa unakosea.

Hata hivyo hivi karibuni nimekutana na jamaa mmoja mwenye tatizo la kuahirisha kama mimi – si unajua inatia moyo kujua hauko peke yako. Halafu karibu kipindi hiki hiki nikakutana na jamaa mwingine aliyenipa ushauri wa kitaalamu juu ya tatizo langu.

Hawa jamaa wawili wamenisaidia kujifunza zaidi juu ya tatizo langu la kuahirisha, kuliangalia kwa mtazamo mwingine na kujipanga kulikabili.

Je, na wewe ni mtu anayepata shida kufanya yale anayotamani kuyafanya, kwa wakati aliokusudia?

Ama ni mtu unayesubiri ‘upate muda’ ili ufanye yale unayoamini yatakupa furaha, kuridhika, n.k.?

Ni mtu unayeahirisha na kupeleka mipango yako ya kufanya mazoezi, kujenga, kumaliza kusoma kile kitabu, kurudi darasani, n.k. mbele kila mara?

Karibu ushirikishe uzoefu wako hapo chini.

Pia karibu uendelee na mfululizo huu kwa kusoma posti inayofuata ili uweze kuliona tatizo hili la kuahirisha kwa mtazamo wa kitaalamu na pia ujue jinsi ya kupambana nalo ili ikusaidie ama imsaidie fulani unayemjua…

0 comments