Jinsi Tabia Inavyoendelezwa

Soma posti hii kwa dakika 4 (makadirio)

‘… in the next 24 hours I will send you my project proposal…’. Hiyo ilikuwa ni sehemu ya email niliyokuwa nimemwandikia mmoja wa wateja wangu watarajiwa.

Alikuwa ni mtu ambaye alisikia juu ya kazi zangu, akanitafuta na hatimaye tukakutana kuongea juu ya jinsi ninavyoweza kutoa huduma hiyo kwa ofisi yake.

Baada ya mkutano huo nilipaswa kuitumia ofisi yake nyaraka mbili; moja kuhusu yale yaliyojiri katika mkutano huo na ya pili kuhusu mahitaji waliyonayo.

Wakati natuma nyaraka hizo ndio nikatoa hiyo ahadi hapo juu, ambayo kwa tafsiri rahisi niliahidi kuwatumia nyaraka nyingine inayoelezea jinsi nitakavyoifanya kazi hiyo, na tena itakuwa ndani ya masaa 24.

Muda natuma ilikuwa ni saa tatu na dakika tisa asubuhi, ikimaanisha nilipaswa kutimiza ahadi yangu kabla ya saa tatu na dakika tisa asubuhi ya siku iliyofuata.

Basi masaa yakaanza kwenda wakati nikifanya mambo mengine; ikawa saa nne, saa tano,… hatimaye saa 11 jioni – muda wa kutoka ofisini, ambapo nikasema acha niwahi kurudi nyumbani ili niandae hiyo project proposal.

Baada ya kufika nyumbani nikaanza kufanya hili, kisha lile, hadi ikafika saa nne usiku; nikasema acha sasa nianze kuandaa hiyo proposal.

Kila nilipokuwa nikijaribu kuanza nikawa nashindwa nianze vipi – maana nilikuwa sijawahi kuandaa nyaraka ya jinsi hii, katika mazingira hayo hapo kabla.

Nikasema acha niingie mtandaoni ili kupata mwongozo, ambapo na hilo halikusaidia sana zaidi ya kuniongezea kazi ya kusoma zaidi – kwa wakati ambao haukuwa mzuri kwangu kusoma.

Mwishowe nikaamua kuahirisha kuandaa hiyo proposal hadi kesho yake. Na badala yake nikasema acha niangalie movie ‘kidogo’. Kwa hiyo nikaishia kuangalia movie, na baada ya hapo nikalala kwa kuchelewa.

Asubuhi yake nikaamka kwa presha ya deadline, nikaanza hiyo kazi, saa tatu ikafika nikiwa bado sijamaliza kuiandaa – kwa hiyo nikaamua liwalo na liwe, nikaendelea kuiandaa hadi nilipomaliza masaa saba baada ya muda nilioahidi 🙁

Stori hii inaelezea jinsi tabia ya kuahirisha inavyokuwa.

Wanasaikolojia wanaamini kuwa ubongo unathamini faida/raha (na unaogopa hasara/madhara) ya sasa zaidi kuliko ile itakayopatikana wakati ujao.

Wakati natoa ahadi nilikuwa namzungumzia ‘James wa wakati ujao’, wakati wa kuiandaa hiyo proposal ulipofika aliyekuwa anahusika ni ‘James wa sasa’; na ilibidi afanye maamuzi juu ya kipi cha kufanya kati ya kuandika proposal itakayoleta faida wakati ujao pale nitakapopewa hiyo kazi na kufanya jambo jingine litakaloleta faida sasa.

Ambapo kama kawaida jibu la ‘James wa SASA’ huwa ni rahisi: kufanya kile kitakacholeta faida sasa.

Hicho ndicho kilichokuwa kinatokea tangu saa tatu asubuhi ya siku nilipotoa ahadi hadi asubuhi ya deadline; ambapo kuandika proposal kulibadilika kutoka kitu kitakacholeta faida wakati ujao na kuwa kitu kitakacholeta HASARA sasa (aibu itakayotokana na kushindwa kutimiza ahadi – kukosa uaminifu).

Lakini hata hivyo nilikuwa nishachelewa!

Kipi Kinafanya Tabia Ijirudie?

Wanasaikolojia wanasema tabia inatengenezwa na matokeo yake.

Kama tabia fulani inaleta matokeo chanya basi itaimarika na itakuwa na uwezekano mkubwa wa kujirudia, na kama inaleta matokeo hasi basi itadhoofika na itakuwa na uwezekano mdogo wa kujirudia.

Mtazamo huu kwa kitaalamu unaitwa ‘Operant Conditioning’ na ulichangiwa na kufanyiwa tafiti kwa kiasi kikubwa na mwanasaikolojia F. B. Skinner.

Ili tabia iimarike lazima itengenezewe mazingira chanya – kitendo kinachoitwa ‘Reinforcement’. Na pia ili idhoofike/iuliwe/iachwe ni lazima itengenezewe mazingira hasi – kitendo kinachoitwa ‘Punishment’.

Mfano wa reinforcement ni kumpa zawadi mwanafunzi baada ya kufaulu mtihani; kwa kufanya hivyo unachochea kujirudia kwa tabia ya kufaulu mitihani.

Mfano wa punishment ni kumzuia mtoto kuangalia TV kila anaposhindwa kumaliza homework yake kwa wakati; kwa kufanya hivyo unajaribu kuua tabia ya kutomaliza homework.

Tukirejea ile stori yetu tuliyoanza nayo utatambua kuwa itakuwa ni vigumu sana kwangu kuacha tabia ya kuahirisha kwa kuwa kila nilipoahirisha nilikuwa natengeneza mazingira chanya kwa tabia hii kuimarika – kila nilipoahirisha nilikuwa nafanya kitu kilichokuwa kinanipa faida/raha ya papo kwa papo, mfano kuangalia movie.

Hivyo nilikuwa naiimarisha tabia hii pasipo hata kujua.

Na kosa hili la kuimarisha/kuchochea tabia tusizozipenda huwa tunalifanya pasipo kujua, karibu kila siku katika maisha yetu ya kawaida : kumpa peremende mtoto anayelia ili anyamaze (tunamzawadia kwa tabia yake ya kulia, hivyo tunaiimarisha); kumwadhibu mtoto mtukutu kila anapokosea (kwa kufanya hivi tunamzawadia umakini wetu – ambao ndio anaoutafuta – na hivyo kuiimarisha tabia yake ya utukutu); n.k.

Je, una tabia zipi ambazo ungependa kuziendeleza/kuziimarisha? Ama kuwa nazo? Kitu cha kufanya ni kuzitengenezea mazingira chanya ya kuendelea, mfano kujizawadia kila unapoifanya.

Na ni zipi ungependa kuziacha – kuondokana nazo, lakini kila ukijaribu unaona haiwezekani?

Jambo la msingi la kufanya ni kuchunguza kipi huwa unafanya ama kinatokea mara tu baada ya tabia hizo; yamkini kitu/vitu hivyo ndio huwa vinaziimarisha tabia hizo kwa kuzitengenezea mazingira chanya ya kuendelea.

Kwa hivyo yamkini unachopaswa kufanya ni tu kuviondoa ama kuacha kuvifanya –  na ikiwezekana kufanya kinyume chake – ili kuweza kuziacha tabia hizo.


Na kwa kuwa posti hii si kila kitu juu ya tabia na utengenezwaji wake, karibu ushirikishe njia unazotumia kuacha tabia usizozitaka – na pia kutengeneza/kuendeleza zile unazozitaka; KARIBU utoe maoni:

0 comments