Chanzo cha Kuahirisha

Soma posti hii kwa dakika 4 (makadirio)

Nianze kwa kukukumbusha kuwa huu ni mwendelezo wa mada tuliyokwishaianza. Hivyo ili uielewe ni vizuri kuanza na sehemu ya kwanza.

Nimekuja kugundua kuwa chanzo cha kuahirisha kufanya kile ambacho nimepanga kwa sehemu huwa ni kuwa na imani potofu kwamba kesho/baadae nitapata muda bora zaidi ama nitakuwa katika mazingira bora zaidi kuliko sasa ya kufanya kile nilichopanga kufanya.

Ni imani potofu kwa kuwa ni kitu kisicho na ukweli wala uthibitisho.

Na hiyo kesho/baadae inapofika huwa natambua kuwa muda haujapatikana na mazingira hayajawa bora kuliko yale ya mwanzo – na tena wakati mwingine huwa yamekuwa duni zaidi.

Matokeo yake huwa naishia kujuta, kuahirisha tena ama kuamua kutofanya jambo hilo kabisa.

Ukweli ni kwamba kama umeshindwa kufanya jambo ulilopanga kulifanya leo kwa sababu umekosa nafasi, hata kesho hautaweza kulifanya.

Kwa nini? Kwa sababu kesho pia ina masaa yaleyale 24 yaliyopo leo, na tena utaratibu na ratiba yako iliyokufanya ushindwe leo na kesho itakuwa ni hiyohiyo – kama haujaamua kuibadili.

Tatizo hili la kuahirisha lilianza kufanyiwa tafiti tangu enzi hizo, miaka mingi kabla ya Kristo. Miongoni mwa watafiti wa enzi hizo walikuwa ni wanafalsafa maarufu wa Kigiriki, Socrates na Aristotle.

Hawa hadi walilipa jina tatizo hili, wakaliita Akrasia. Tafsiri yake isiyo rasmi ni hali ya mtu kufanya jambo tofauti na lile analoamini kuwa ni sahihi kwa wakati na mazingira aliyomo.

Kitu hicho ndicho kinachotokea mtu anapoahirisha: kwamba mara zote unapoahirisha kufanya kile ulichopanga, huwa unafanya kitu kingine – ambacho haukuwa umepanga – badala yake, mfano kuangalia movie wakati uliopanga kufanya mazoezi, kulala muda uliopanga kumalizia kusoma kile kitabu, n.k.

Saikolojia Inasemaje Juu ya Kuahirisha ?

Wanasaikolojia wanasema tatizo hili linasababishwa na kitu wanachokiita ‘Time Inconsistency’ ama kwa tafsiri isiyo rasmi ‘Mgongano wa Muda’: Hali ya jambo kuwa na thamani tofauti – machoni mwa mfanya maamuzi – wakati wa kupanga ukilinganisha na wakati wa kulitekeleza.

Hii inatokana na ubongo kuthamini mambo yanayoleta faida – raha, furaha, kuridhika, n.k. – kwa haraka (sasa) ukilinganisha na yale yanayoleta faida baadae.

Wanasema ubongo huwa na sehemu mbili zinazohusika na maamuzi ya jambo.

Sehemu ya kwanza kazi yake huwa ni kuhakikisha mwili haupatwi na adha, maumivu ama hali yoyote mbaya. Huwa ni kuhakikisha mwili unapata raha. Sehemu hii huwa inajali muda huu wa ‘sasa’ na umakini wake wote huwa upo kwenye hii ‘sasa’.

Sehemu ya pili huwa na kazi ya kumsaidia mtu kufanya maamuzi sahihi kwa kuchukua yaliyoko kwenye mazingira ya sasa, kuyalinganisha na yale aliyowahi kukutana nayo zamani, na kisha kumsaidia kufanya uchaguzi wa nini cha kufanya na cha kutofanya ili aweze kuifikia ile kesho anayoitamani.

Kwa kuwa sehemu hii ya pili ndio yenye mtazamo mpana zaidi – tofauti na ule finyu wa sehemu ya kwanza wa kuangalia ‘sasa’ pekee – maamuzi sahihi yote huwa yanatoka hapa; maana huwa inamwezesha mtu kufanya maamuzi sasa kwa ajili ya sasa na kesho, akitumia uzoefu na yale aliyojifunza jana.

Sehemu hii huwa inajali zaidi kesho, na umakini wake huwa upo kwa ajili ya kesho.

Sasa wakati mtu anapanga jambo sehemu ya pili ndio ina nguvu (iliyo katika udhibiti) kwa kuwa jambo hilo huwa ni kwa ajili ya wakati ujao – kwa ajili ya kesho.

Kwa hiyo sehemu hii huwa inaipa mipango hiyo thamani kubwa. Hivyo mtu anapanga akiamini kabisa muda ukifika atatekeleza.

Hata hivyo unapofika muda wa utekelezaji sehemu ya kwanza ndio huwa kwenye usukani, kwa kuwa ndio inayoshughulika na ‘sasa’.

Na kwa kuwa jambo lililopangwa faida yake haipo sasa bali kesho – wakati ujao – basi sehemu hii hulipa thamani ndogo jambo husika.

Matokeo yake lile jambo ulilolipanga kwa matarajio makubwa na kuliona lina umuhimu unaishia kuliona halina umuhimu tena, ukililinganisha na yale mambo unayoamua kufanya badala yake – baada ya kuliahirisha mfano kuangalia movie ama kulala; kwa nini? Kwa kuwa mambo hayo yanaleta faida/raha ya haraka – ya sasa – kwa mwili na hivyo yanapewa thamani kubwa na ile sehemu ya kwanza.

Hebu tuzungumze kwa mfano:

Umeahirisha kufanya mazoezi na badala yake ukaangalia movie


Labda umepanga kufanya mazoezi kila siku kwa saa moja – kuanzia saa moja hadi saa mbili usiku.

Maamuzi ya mpango huu yamekuja baada ya sehemu ya pili ya ubongo kutumia taarifa ulizojifunza juu ya faida za kiafya za kufanya mazoezi – faida ambazo utazipata hapo mbeleni baada ya kuwa na mazoea hayo.

Wakati unapanga, sehemu ya pili ya ubongo inalipa jambo hili thamani kubwa; unaliona ni jambo muhimu kufanya.

Masaa yameenda hatimaye imefika saa moja usiku – muda wa kutekeleza mpango wako wa kufanya mazoezi.

Hata hivyo ile sehemu ya kwanza ya ubongo ndio iliyoko kwenye usukani kwa sasa, na kama kawaida lengo lake ni moja tu – kuhakikisha mwili unapata faida/raha, tena muda huu – SASA.

Sehemu hii haijui habari ya jana, haihitaji kujua taarifa juu ya faida za mazoezi, tena haina mpango wa kujishughulisha na mambo yajayo, ya kesho; yenyewe inachojali ni muda huu – SASA pekee.

Kwa hiyo mpango wa kufanya mazoezi unakuwa hauna thamani tena. Badala yake, kuangalia movie ndio kunaonekana kuwa na thamani kubwa; kwa kuwa kunaupa mwili RAHA, tena SASA.

Matokeo yake mtu anaahirisha kufanya mazoezi, anaamua kuangalia movie. Thamani ya kufanya mazoezi katika muda wa kupanga imekuwa tofauti na thamani ya kufanya mazoezi katika muda wa utekelezaji – ‘Time Inconsistency’.


Endelea kuwa nami katika sehemu inayofuata, ambayo ni ya mwisho ya mfululizo huu ili tujifunze pamoja jinsi ya kushinda tatizo la kuahirisha.

Na najua una cha kuchangia, sehemu ya comments hapo chini ni kwa ajili hiyo, KARIBU…

0 comments